-Afisa habari wa Klabu ya Yanga SC, Hassan Bumbuli amesema Nahodha wa klabu ya Yanga Papy Tshishimbi amewasili jana nchini kujiunga na kikosi cha Yanga kujiandaa na mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam hapo kesho. Papy alipewa mapumziko na alienda kwao DR Congo baada ya mchezo wa watani wa jadi January 04.

-Aliyekuwa kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Meck Mexime amethibitisha kukamilisha mchakato wa kujiunga na Yanga kama kocha msaidizi

Hata hivyo, amesema kuwa kwa sasa bado yuko na klabu yake na kwamba, baada ya kukamilisha baadhi ya taratibu ataweka hadharani ni wakati gani atajiunga na mwajiri wake mpya.

Mexime, ambaye amepeleka kilio Jangwani kwa kuwafunga bao 3-0 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, amesema amefanya mazungumzo na mabosi wa Yanga, lakini bado haijawa wazi muda wa kuanza majukumu hayo mapya hadi taratibu zingine zitakapokamilika.

“Kuhusu kutambulishwa leo hapana sio kweli, nipo njiani na timu tunakwenda Kagera na tumeanza safari jana Alhamisi kutoka Dar es Salaam. Mambo yakikamilika nitarejea Dar es Salaam kwa hatua zingine zaidi,” alisema.
Wakati huohuo, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela ameweka wazi kuwa wameshindwa kumtambulisha Mexime leo Ijumaa kama walivyopanga kutokana na kutokamilika baadhi ya taratibu.

“Kwa upande wa Mexime tumemalizana na kilichobaki na uongozi wa Kagera Sugar ambao, bado wana mkataba naye wa miezi sita hivyo mazungumzo baina yetu yakikamilika basi muda wowote atatambulishwa na kuanza kazi Jangwani,” alisema.

Kwa upande wa Charles Boniface mkwasa, yeye atabadilishiwa majukumu na kuwa mkurugenzi wa ufundi wa Klabu ya Yanga.